* * *
[Pope John Paul II’s Year 2004 Message for World Mission Sunday (24 October, 2004)
on the theme «Eucharist and Mission»]
UJUMBE WA BABA MTAKATIFU YOHANE PAULO II
KWA AJILI YA JUMAPILI YA MISIONI DUNIANI
(24 Oktoba, 2004)
Mada: “Ekaristi na Misioni”
Wapendwa sana Kaka na Dada zangu!
Kazi ya Kimisionari ya Kanisa ni muhimu mwanzoni mwa Milenia ya Tatu
1. Kazi ya Kanisa ya Umisionari Mwanzoni mwa Milenia ya tatu ni yenye umuhimu mkubwa kama niliyokwisha kusema mara nyingi. Kama nilivyo taja katika Ensiklika “Redemptioris Missio” (Utume wa Mkombozi) umisionari ndio bado unaanza nasi yatupasa kujitosa kwa moyo wote kwa ajili ya huduma yake (rej. 1). Taifa lote la Mungu katika kila hatua ya hija yake katika historia yake linaitwa kushiriki “kiu” ya Mkombozi (rej. Yn 19:28). Kiu hiyo ya kuokoa roho za watu daima imekuwa ni mang’amuzi mazito ya watakatifu. Inatosha kumfikiria, kama mfano, Mt. Teresia wa Lisieux, Msimamizi wa Misioni na Askofu Komboni, mtume mkubwa wa Afrika ambaye hivi karibuni nilipata furaha ya kumwinua kwa heshima ya altareni.
Changamoto za kijamii na za kidini zinazowakabili wanadamu katika zama zetu zinawataka waamini kuchochea hamasa yao ya umisionari. Ndiyo! Ni lazima kuzindua tena utume “kwa mataifa” kwa ushujaa, kuanzia na utangazaji wa Kristo, Mkombozi wa kila mtu. Kongamano la Kimataifa la Ekaristi litakaloadhimishwa Guadalajara – Mexico mwezi ujao wa Oktoba, itakuwa fursa ya pekee kabisa ya kukua katika utambuzi wa pamoja wa kimisionari kandokando ya Meza ya Mwili na Damu ya Kristo.
Kanisa, linapoiizunguka altare, linatambua vizuri zaidi asili yake na mamlaka yake ya umisionari. Kama mada ya Jumapili ya kiulimwengu ya Misioni ya mwaka huu inavyosisitiza bayana “Ekaristi na Misioni” haviwezi kutenganishwa. Licha ya tafakari kuhusu kiungo kilichopo kati ya fumbo la Ekaristi na fumbo la Kanisa, mwaka huu kutakuwa na rejea nzuri kabisa kwa Bikira Maria Mwenye heri kwa sababu ya tukio la mwaka wa 150 wa tangu kutajwa dogma ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili (1854-2004). Na tutafakari Ekaristi kwa macho ya Maria. Tukitegemea maombezi ya Bikira Mwenye heri, Kanisa linamtolea Kristo, mkate wa wokovu, kwa watu wote, ili waweze kumtambua na kumpokea kama Mwokozi pekee wa mwanadamu.
Utume wa Kanisa unachota nguvu ya kiroho kwa kushiriki Mwili wake na Damu yake
2. Nikirejea kimawazo ghorofani katika Chumba cha juu karamu ya mwisho mwaka jana siku ya Alhamisi Kuu nilitia saini Ensiklika “Kanisa la Kiekaristi” (Ecclesia de Eucharistia) na toka humo napenda kuchukua sehemu kadhaa ambazo zitatusaidia, wapendwa wangu kaka na dada, kuiishi Jumapili ya Missioni ya duniani mwaka huu kwa roho ya Kiekaristi. “Ekaristi inaunda Kanisa na Kanisa linaitengeneza Ekaristi” (n. 26), niliandika, nikiangalia namna gani utume wa kimissioni wa Kanisa ni mwendelezo wa utume wa Kristo (rej. Yn 20:21) na huchota nguvu ya kiroho kutokana na ushirika wa Mwili wake na wa Damu yake. Lengo mahususi la Ekaristi hasa ni “muungano wa watu na Kristo na ndani yake na Baba na Roho Mtakatifu” (Ecclesia de Eucharistia, n. 22). Tunaposhiriki Sadaka ya Ekaristi Takatifu tunatambua kwa kina zaidi kwamba ukombozi ni kwa ajili ya watu wote, na hivyo umuhimu wa utume wa Kanisa pamoja na programu zake, “ambao una kiini chake katika Yesu Mwenyewe, ambaye anatakiwa ajulikane, apendwe na kufuaswa ili ndani yake tuishi maisha ya Utatu Mtakatifu na pamoja naye tuigeuze historia mpaka utimilifu wake katika Yerusalemu ya mbinguni (Ecclesia de Eucharistia, n. 60).
Tukimzunguka Kristo katika Ekaristi Takatifu Kanisa linakua kama taifa, hekalu na familia ya Mungu: Moja, Takatifu, Katoliki na la Kitume. Papo hapo unafahamu vizuri zaidi hali yake ya Sakramenti ya wokovu kwa ajili ya wote na ukweli unaoonekana ukiwa na muundo kwa kihiararkia. Kwa yamkini “hakuna jumuiya ya Kikristo inayoweza kujengwa kama haina msingi na kiini katika adhimisho la Sakramanti Kuu ya Ekaristi” (Ecclesia de Eucharistia, n. 33; Presbyterorum Ordinis, n. 6). Mwishoni mwa kila Misa Takatifu, padre anayeongoza ibada anapowaaga washiriki akisema “Nendeni na amani” wote wajisikie kuwa wanatumwa kama “wamisionari wa Ekaristi” kupeleka katika mazingira yote zawadi kubwa waliyoipokea. Kwa yamkini, yeyote anayekutana na Kristo katika Ekaristi Takatifu hawezi kuacha kutangaza upendo wenye rehema wa Mkombozi kwa njia ya maisha yake.
Hitaji la mitume ambao ni “bingwa” na mashahidi katika adhimisho la, kuabudu na kutafakari Ekaristi Takatifu
3. Ili kuishi Ekaristi Takatifu ni muhimu na pia yatupasa kutumia muda mwingi mbele ya Sakramenti kuu kuabudu, jambo ambalo mimi mwenyewe ninalionja kila siku ninachota humo nguvu, faraja na msaada (ref. Ecclesia de Eucharistia, n. 25). Mtaguso wa Pili wa Vatikano unathibitisha kwamba, Ekaristi ni “Chemchemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo” (Lumen Gentum, n. 11), “chemchemi na kilele cha uinjilishaji wote” (Presbyterorum Ordinis, n. 5).
Mkate na divai, kazi ya mikono ya wanadamu, vilivyogeuzwa, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, kuwa Mwili na Damu ya Kristo, vinakuwa amana ya “mbingu mpya na dunia mpya” (Ufunuo 21:1), inayotangazwa na Kanisa katika utume wake wa kila siku. Katika Kristo, ambaye tunamwabudu akiwa katika fumbo la Ekaristi Takatifu, Baba alitamka neno lake la mwisho kuhusiana na mwanadamu na historia ya mwanadamu.
Kanisa lingewezaje kutekeleza wito wake bila kujenga uhusiano wa kudumu na Ekaristi Takatifu, bila kujilisha na chakula hiki kinachotakatifuza, bila kujenga utendaji wake wa kimisionari juu ya msaada huu wa lazima kabisa. Ili kuweza kuuinjilisha ulimwengu kuna haja ya kuwepo kwa mitume “bingwa” na mashahidi katika kuadhimisha, kuabudu na kutafakari Ekaristi Takatifu.
Waamini hujaliwa kutambua kwamba kazi ya umisionari ni kuwa “sadaka yenye kibali kama toleo, ikishatakaswa na Roho Mtakatifu”
4. Katika Ekaristi Takatifu tunaliweka hai fumbo la Ukombozi linalofikia kilele katika sadaka ya Bwana, kama inavyotamkwa katika maneno ya konsekrasio: “Mwili wangu utakaotolewa kwa ajili yenu…. Damu yangu itakayomwagika kwa ajili yenu” (Luka 22:19-20). Kristo alikufa kwa ajili ya wote; na kwa ajili ya wote anakuwa zawadi ya wokovu ambao Ekaristi Takatifu inaifanya mithili ya Sakramenti uwepo wake katika mwendo wa historia: “Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi” (Luka 22:19). Amri hiyo wanakabidhiwa wahudumu walioamriwa kwa njia ya Sakramenti ya Daraja Takatifu. Watu wote wanaalikwa kwenye karamu hii ili waweze kushiriki katika uzima ule ule wa Kristo. “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi” (Yn 6:56-57). Wakilishwa Naye waamini wanajaliwa kutambua kwamba kazi ya umisionari ni “kuwa sadaka yenye kibali, ikishatakaswa na Roho Mtakatifu” (Rum 15:16), ili kuwa zaidi na zaidi “moyo mmoja na roho moja” (Mdo 4:32) na kushuhudia upendo wake hadi mwisho wa dunia.
Kanisa, Taifa la Mungu, linaposafiri katika karne, nakurudia tena na tena kila siku Sadaka ya Altare, linangojea ujio wa Kristo katika utukufu. Hilo linatangazwa baada ya konsekrasiyo na Jamii inayoadhimisha, inayoizunguka altare ikiadhimisha sadaka ya Ekaristi. Tena na tena kwa imani iliyotiwa nguvu mpya Kanisa hurudia tamaa yake ya kukutana hatimaye na Yule anayekuja kuleta utimilifu wa mpango wake wa kuwaokoa watu wote.
Roho Mtakatifu akitenda kazi bila kuonekana, lakini kwa nguvu, anaongoza taifa la Kikristo katika hija hii ya kiroho ambamo kwa hakika wanapambana na magumu na wanaonja fumbo la Msalaba. Ekaristi Takatifu ni kitulizo na amana ya ushindi wa mwisho kwa wale wanaopambana na uovu na dhambi. Ni “mkate wa uzima” unaowashikilia wa
le ambao Nao, kwa zamu yao, wanakuwa “mkate uliomegwa” kwa ajili ya wengine wakilipia maisha yao hata kwa kifodini uaminifu wao kwa Injili.
Fursa ya kuimarisha juhudi yao ya kimisionari
5. Mwaka huu, kama nilivyokwishadokeza, itakuwa ni kumbukumbu ya mwaka wa 150 tangu dogma ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili ilipotangazwa. Maria “alikombolewa kwa namna ya pekee na ya hali ya juu kwa sababu ya mastahili ya Mwana wake” (Lumen Gentium, n. 53). Nilisema katika Ensiklika “Ecclesia de Eucharistia”: Tunapomtazama Maria, tutajaliwa kujua nguvu ile inayogeuza iliyomo katika Ekaristi Takatifu. Ndani ya Maria tunauona ulimwengu ukifanywa upya katika pendo” (n. 62).
Maria, “tabernakulo” ya kwanza katika historia” (n. 55) anatuonyesha na anatupatia Kristo aliye Njia, Ukweli na Uzima (rej. Yn 14:6). Kama Kanisa na Ekaristi Takatifu vinavyounganika hivi bila kutengana, hayo hayo lazima yasemwe juu ya Maria na Ekaristi Takatifu” (Ecclesia de Eucharistia, n. 57).
Natumaini kule kuingiliana kwa furaha kwa Kongamano la Kimataifa la Ekaristi na kumbukumbu ya miaka 150 ya tangazo la dogma ya Bikira Maria Kukingiwa Dhambi ya Asili, kutoe kwa waamini, parokia, na asasi za kimisionari fursa ya kuimarisha juhudi zao za kimissionari ili katika kila jumuiya iwepo daima “njaa ya kweli kwa ajili ya Ekaristi Takatifu (Ecclesia de Eucharistia, n. 33).
Hii pia ni fursa nzuri kutaja mchango unaotolewa kwa ajili ya utume wa Kanisa. Ninaviweka vyama hivyo kwa upendo moyoni mwangu na ninavishukuru, kwa niaba ya wote, kwa ajili ya huduma zao nzuri zinazotolewa kwa ajili ya uinjilishaji na utume “kwa mataifa”. Ninawaomba nanyi kuvisaidia vyama hivyo kiroho na kwa hali a mali ili kwa njia ya mchango wao utangazaji wa Injili uweze kuwafikia watu wote wa hapa duniani.
Kwa hisia hizo, kwa maombezi ya Kimama ya Maria, “Mwanamke wa Ekaristi”, kwa furaha ninawapa Baraka yangu ya Kitume.
Kutoka Vatikano, 19 Aprili 2004
Yohane Paulo II